
MWENYEKITI wa UVCCM, Mkoa wa
Arusha,kwa miaka mitano, James Ole Millya,ametangaza kujiuzulu nafasi
zote kuanzia Taifa hadi Mkoa na kutangaza kujiunga na Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa madai kuwa CCM imefilisika
kimawazo na haitoi matumaini kwa watanzania.
Aidha alisema hawezi
kuendelea kupanda gari lenye pancha lukuki, hivyo ameamua kupanda gari
lisilo na pancha na lenye kutoa matumaini mapya kwa watanzania.
Hayo ameyasema leo,
wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Kibo Palace,
iliyopo Jijini hapa. Amesema mara nyingi alikuwa akikemea mambo ambayo
yanaweza kubomoa chama cha CCM kwa upendo, lakini alikuwa akipuuzwa kwa
sababu ya chama hicho kuwa na kikundi cha wenyewe.
“Mimi nanukuu maneneo
ya Nyerere kuwa alishawahi kusema CCM sio mama yangu na mimi pia CCM
sio mama yangu na natangaza rasmi, kuondoka ndani ya chama hiki na
najiunga na Chadema, sababu ndicho chama chenye kuleta tumaini jipya
kwa watanzania,”alisema.
Ametaja nafasi
alizoachia ngazi ni pamoja na Mjumbe kamati ya utekelezaji UVCCM Taifa,
Mjumbe kamati ya siasa Mkoa na Mjumbe Halmashauri Kuu CCM Mkoa.
Amesema kuwa
inasikitisha kuona Vijana wa UVCCM Mkoa wa Pwani, wanatoa matamko kuwa
Rais ajaye 2015 hatatoka kanda ya Kaskazini na anayemfahamu ni Rais
peke yake ambaye ni Jakaya Kikwete.
Millya alisema cha
kusikitisha pale alipokemea kauli hiyo alipuuzwa na hadi sasa Ikulu
haijawahi kutoa kemeo kwa Vijana hao na wala kukataza kauli hizo
kutolewa, jambo lililompa jibu kuwa Ikulu inahusika kwa namna moja au
nyingine na kauli hiyo.
Aidha alisema kuna
Vijana wengi walioko ndani ya CCM wakiishi kwa matumaini ya kusubiri
kuteuliwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya kama sio Mkoa, ila yeye hawezi
kuishi kwa matumaini kama muathirika wa Ukimwi.
Hata hivyo alitoa
wito kwa Vijana wote wenye nia ya dhati na mapenzi mema ya nchi yao,
kumfuata Chadema ambako kunatoa tumaini jipya la maisha ya watu.
Millya ambaye
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM tangu 2008 hadi sasa,
aliwashukuru vijana kwa kumpa ridhaa hiyo na ataendelea kuwashukuru,
ila ameamua kwa ridhaa yake kuachia ngazi zote kwa ajili ya ukombozi wa
kweli.
Millya hivi karibuni
alijitosa kinyang’anyiro cha kugombea Ubunge wa Afrika Mashari ndani ya
Chama chake cha CCM, lakini alichijiwa baharini na kutolewa jina lake.
No comments:
Post a Comment