Wednesday, August 17, 2011

Wanaokula hadharani, kuvaa nguo fupi Zanzibar kukiona




 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imelitaka Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaokula hadharani na kuvaa nguofupi wakati huu wa mfungo mtukufu wa Ramadhani.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema serikali imeamua kutoa agizo hilo baada ya kujitokeza baadhi ya watu kuonekana wakila mchana hadharani na baadhi ya vijana kuonekana wakiwa wamelewa na kuranda mitaani kinyume na misingi ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Aidha, alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakionekana mitaani wakiwa wamevaa nguo zisizokuwa na heshima.
Waziri Aboud amesema kwamba baadhi ya migahawa na nyumba za kulala wageni zimekuwa zikitoa huduma mchana katika kipindi cha Mwezi Mtukufu. Waziri Aboud alisema kimsingi wananchi hawazuiwi kula mchana kulingana na imani zao, lakini wanatakiwa kufanya hivyo wakiwa katika maeneo ya faragha kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawataka wale wote wanaojishirikisha na vitendo hivyo waache mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria pamoja na kwenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na mafundisho yake Mtume Mohammad,” alisema.
Aidha, alisema serikali inatarajia wananchi wote Unguja na Pemba watashirikiana kurudisha heshima ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Waziri Aboud amesema serikali imeamua kutoa tamko hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka Jumuiya moja ya kidini Zanzibar juu ya kuwepo watu wanaokula mchana na kuvaa nguo fupi bila kuzingatia misingi ya mfungo wa Mwezi wa Ramadhani.
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment