Monday, August 1, 2011

JE TUTAFIKA?

Wanafunzi wachangishwa kununua chaki
 WILAYA ya Muleba mkoani Kagera imekumbwa na ukosefu mkubwa wa chaki za kuandikia ubaoni, hasa kwa shule za msingi. Hatua imesababisha walimu kuchangisha wanafunzi fedha za kununulia vifaa hivyo, huku wengine wakishindwa kufundisha kwa kuandika ubaoni kutokana na tatizo hilo.
Hali hiyo ilibainika juzi katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na swali la Diwani wa Bisheka, Steven Tibanyekomya, ambaye alitaka kujua ni hatua gani zimechukuliwa na uongozi wa Halmashauri kupitia Idara ya Elimu kutatua tatizo hilo ambalo linaonekana kuwa kero kubwa wilayani hapa.
Alisema katika utafiti wake kwenye kata yake na maeneo mengi ya wilaya hii, shule nyingi hazina chaki kwa mwezi sasa, hatua ambayo wakati mwingine imekuwa ikisababisha walimu kutofundisha kwa kuandika ubaoni na hivyo kuwanyima wanafunzi haki ya msingi ya kupata elimu.
“Hii hali kwa kweli ni aibu kwetu viongozi na Serikali kwa jumla, kwa sababu haiingii akilini, kwamba chaki zinakosekana shuleni na kufanya wanafunzi washindwe kusoma, sasa mimi nataka Halmashauri inieleze kama inalijua jambo hili na kama ndivyo ni hatua gani zimechukuliwa mpaka sasa? Lakini pia kuna mikakati ipi ya kuhakikisha kwamba hali kama hii haiwezi kujitokeza tena?’’ Alihoji Steven.
Aliongeza kuwa katika baadhi ya shule, walimu wamekuwa wakilazimika kuchangisha wanafunzi kati ya Sh 100 na Sh 200, ili kununulia chaki kwa madai kuwa hakuna ruzuku zinazopelekwa shuleni kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo ya ununuzi wa chaki.
“Sasa kwa hali kama hii tuliyofikia kwenye wilaya yetu ya wanafunzi kuchangishwa fedha za kununulia chaki, vitu ambavyo tulikwishaondokana navyo miaka mingi iliyopita, sijui elimu yetu tunaipeleka wapi! Wazazi wanalalamika kuhusu michango lakini hatuwezi kulaumu walimu … wafanye nini?...’’ alisema na kuhoji Diwani huyo.
Akijibu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Oliver Varunge, ambaye ana wiki moja tu tangu ashike wadhifa huo wilayani hapa, alionekana kushangazwa na madai hayo na kumtaka aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu Pastory Kajuna ambaye pia ni Ofisa Elimu ya Msingi wilayani hapa, kujibu madai hayo.
Kajuna alikiri kuwapo ukosefu mkubwa wa chaki shuleni na kueleza kuwa hali hiyo inasababishwa na ukosefu wa ruzuku shuleni, ambayo imekuwa haitolewi na Serikali ama kutolewa kidogo sana tofuti na wakati uliopita.
“Ni kweli hilo tatizo lipo na ni kubwa tunalifahamu … lakini tatizo kubwa hapa ni ukosefu wa ruzuku … inakuja kidogo sana, ambayo haitoshelezi, lakini pia kibaya zaidi ni kwamba hata hicho kidogo kinachokuja kinacheleweshwa, lakini tunashukuru kuna fedha zimekuja juzi hivi karibuni Sh milioni 26, tumeamua kuzielekeza katika kupunguza tatizo hilo, kwa sababu bado hazitoshi,’’ alisema Pastory.
Aliongeza kuwa Wilaya kupitia Idara ya Elimu ya Msingi iko katika mchakato wa kuhakikisha tatizo hilo linamalizika, ili kuondoa usumbufu uliopo hivi sasa kwa walimu, wanafunzi na wazazi, hali ambayo inaweza kusababisha kushuka kwa kiwango cha ufundishaji na hivyo elimu kushuka.

 Source:Habari Leo

No comments:

Post a Comment