 |
Polisi ACP Msangi |
|
|
|
|
|
ASKARI anayetuhumiwa kumteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, Kamishna wa Polisi Msaidizi (ACP), Ahmed
Msangi, amehojiwa na kuzungumzia kilichotokea kuhusiana na tuhuma
kwamba aliambiwa arejeshe simu ya mkononi na pochi ya Dk. Ulimboka.
Akizungumza
na Gazeti la JAMHURI, ACP Msangi alikiri kwenda katika wodi ya wagonjwa
mahututi katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa nia ya kumhoji
Dk. Ulimboka, ila akaeleza mshangao wake kutokana na habari
zilizochapishwa mwishoni mwa wiki, kuwa aliambiwa arejeshe pochi na simu
ya Dk Ulimboka kwa maana kuwa alivipora walipomteka.
Vyombo vya
habari mwishoni mwa wiki vilichapisha taarifa bila kutaja jina la
askari anayetuhumiwa, lakini pia ukawa unasambazwa ujumbe mfupi kupitia
simu za mkononi ambao ulisema hivi:
“Kamanda Msangi aliyemkamata
na kumtesa Dr. Ulimboka, yuko katika jopo la kuchunguza nini kilimtokea
Dk. Ulimboka. Alipofika kumhoji Dk. Ulimboka alimwambia ‘Nirudishie
simu na wallet yangu’. Kamanda Msangi taratibu akaondoka wodini kichwa
chini. Kama wewe ni mpenda haki na unapinga ujinga na dhuluma, watumie
ujumbe huu watu wengi kadri uwezavyo ili wamjue dhalimu aliyeongoza
unyama huu,” ulisema ujumbe huo unaosambazwa kupitia simu za mkononi.
Tume
ya Jeshi la Polisi iliyoundwa kuchunguza tukio la Dk. Ulimboka kutekwa
nyara, kwa mujibu wa Kamanda Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, inaongozwa na Kamanda Msangi.
Kamanda Msangi (pichani)azungumza
Jamhuri: Afande
umetangazwa kuongoza hii Tume ya Polisi kuchunguza suala la Dk.
Ulimboka, lakini taarifa zilisosambaa zinaonyesha Ulimboka alikwambia
umerejeshee simu na wallet yake. Unalizungumziaje hili?
Kamanda Msangi: Hata
mimi nimesikia hizi taarifa, na zimenisikitisha mno. Naamini taarifa
hizi zina malengo ya ziada. Si kweli kwamba nilishiriki kumteka Dk.
Ulimboka na wala sijawahi kuwa na wazo hilo.
Jamhuri: Ikiwa hukushiriki kumteka iweje wodini akwambie nirudishie simu yangu?
Msangi: Kwanza
ifahamike mimi huyu Dk. Ulimboka na mwenzake Dk. Deo nimewafahamu siku
nyingi sana. Kwa maana hiyo ni mtu anayenifahamu vizuri tu. Kuna
upotoshaji wa makusudi umefanywa ambao mimi nadhani una msukumo wa
kisiasa.
Alichosema Dk. Ulimboka nilipozungumza naye, ni kwamba
simu moja ilidondoka, nyingine wale watu waliomteka wameichukua pamoja
na wallet yake. Hivyo alikuwa ananitajia vitu vilivyopotea.
Nilipomuuliza iwapo anakumbuka namba ya simu, aliniambia nikamuulize Dk.
Deo. Sasa nashangaa mtu aliyepenyeza uongo huu kwamba alisema mimi
ndiye niliyempora hivyo vitu… sielewi ni nani na ana malengo gani.
Jamhuri: Haya unayasema wewe, hivi unadhani jamii itakuamini kwa kauli hizi, haitaonekana unajitetea tu?
Msangi: Wakati
anazungumza maneno haya, alikuwapo Profesa Museru ambaye ni Mkurugenzi
wa MOI. Sina cha kuficha kamuulize tu, atakwambia alichosema Dk.
Ulimboka. Yupo pia Dk. Deo, huyu ananifahamu na Dk. Ulimboka anasema
walikuwa wote wakati anatekwa. Dk. Deo ananifahamu, akaulizwe iwapo mimi
ndiye niliyemteka Dk. Ulimboka.
Jamhuri: Tuhuma hizi zilianza kusambaa mapema tu Ijumaa. Je, wewe hukuwa na hofu kwenda pale MOI kumhoji Dk. Ulimboka?
Msangi: Ndugu
yangu, nchi hii ina askari wengi mno. Hivi mimi kwa akili ya kawaida
naweza kushiriki kumteka Dk. Ulimboka kisha nikaenda wodini kumhoji?
Hata katika akili ya kawaida ya binadamu hilo haliwezekani.
Jamhuri: Hizi
tuhuma zilizoelekezwa kwako ni nzito. Wewe ndiye uliyeteuliwa kuongoza
Tume ya Uchunguzi wa tatizo hili. Je, unadhani uchunguzi utakaofanya
utaaminiwa na wananchi ukitoa ripoti?
Msangi: Mimi
ninachokuhakikishia sikushiriki kumteka na si kweli kwa kila hali. Mambo
kama haya yanakatisha tamaa. Kama tunaanza kuzushiana uongo kwa kiwango
hiki, nchi hii sijui inaelekea wapi! Kimsingi imenikatisha tamaa mno.
Wapo wanaosema nijiuzulu katika Tume hii lakini mimi nasema wakubwa
wangu wamenipa kazi hii na watakaloamua nitalipokea.
Hivi wewe
gazeti lako likituhumiwa unaacha kuendelea kutafuta habari? Nitaendelea
kufanya kazi hii kama nilivyoapa siku nilipohitimu mafunzo kwamba
nitalitumikia taifa kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu katika kiapo
changu cha utii. Na hilo ndilo nitakaloendelea kufanya. Watu wanapenda
kuharibiana maisha tu.
Profesa Museru asema alichokisikia
Habari hizi zimechapishwa na Gazeti la Jamhuri